Saturday, September 10, 2011

KITABU CHA MWANZO 1-11


               



 


ALIYOMO

UKURASA
1.0 Utangulizi wa Kitabu cha Mwanza ………….
1.1 Mazingira ya Sura 1—11 ………………………..
1.2 Uandishi …………………………………………………..
1.3 Mtindo wa Uandishi ………………………………..



2.0 Sura ya Kwanza - Tatu…………………………...
2.1 Muhtasari wa sura 1—3…………………………..
2.2 Mafafanuzi………………………………………………..
2.2.1 Baraka za Mungu………………………………….
2.2.2 Mungu na miungu………………………………..
2.2.3 Mfano wa Mungu…………………………………..
2.2.4 Mazingira……………………………………………….
2.2.5 Wajibu wa mwanadamu……………………….
2.2.6 Ndoa……………………………………………………..
2.2.7 Ufalme wa Mungu…………………………………



3.0 Muhtasari wa Sura ya Nne - Tano…………..
3.1 Kuanza kwa ustaarabu…………………………...
3.2 Uzao wa Kaini…………………………………………..
3.3 Uzao wa Seth…………………………………………..



4.0 REHEMA NA HUKUMU YA MUNGU…………..

4.1 Gharika…………………………………………………..

4.2 Laana na Baraka……………………………………...

4.3 Mnara wa Babel (Lugha mbalimbali)……….

4.4 Utangulizi wa Mababa wa Imani……………..


JINA LA KOZI; AGANO LA AKALE: MWANZO 1-11
NO. KOZI BT205
Lengo kuu:
·    Kosi itamsaidia mwanachuo kuelewe mafundisho 
   muhimu katika Mwanzo 1-11, Kuhubiri na kubadili
   maisha yake.
  Lengo Mahususi:
   Mwisho wa kosi mwanchuo atakuwa anao uwezo wa;
·    Kuelezea kitusi cha Mwanzo 1-11
·    Kufanya mhutasari wa mafundisho yapatikanayo katika
   sura hizi.
·    Kuoanisha sura hizi na sehemu zingine za Agano  
   Jipya.
·    Kumwelezea Yesu katika Agano la Kale.
·    Kutumia Agano la Kale kama msingi wa mahubiri.

KAZI
          Mwanachuo anatakiwa kuhudhuria na kushiriki  darasani kwa jumla ya saa 30 kwa kukutana ana kwa ana na mkufunzi. Saa 15 kwa ajili ya kufundishana   wenyewe
Mwanachuo ataandika insha mbili kila moja itakuwa na alama 10.
          Kutakuwepo majaribio 2. moja itakuwa jaribio la wazi lenye alama 15. Jaribio ficho litakuwa na alama 10 Alama 5 zitahusika na mahudhurio na ushiriki darasani.
Mwanachuo anatakiwa kupata alama zisizopungua 20 ili kupata kibari cha kufanya mtihani wa semester.


UTANGULIZI

          Biblia ni kitabu cha vitabu sitini na sita. Biblia imegawanyika katika sehemu kuu mbili: Agano la Kale na Agano Jipya. Ingawa biblia haikutumika katika mfumo huu wa leo lakini sehemu kubwa ya vitabu vya Agano la Kale vimetumika kabla ya Kuzaliwa kwa Kristo.
          Kusudi la Agano la Kale ni kuonyesha kumbukumbu namna Mungu alivyohusika na taifa la   Israel katika misingi ya kimaagano ambayo alifanya nao katika vipindi mbalimbali. Habari za awali kabisa za Agano la Kale zinaelezea kazi Mungu ya Uumbaji, anguko, na gharika.
          Katika maisha ya Israel na kanisa leo, sura ya 1-11 ya kitabu cha Mwanzo ni za muhimu sana. Sura hizi ndizo zimebeba misingi ya imani yetu, kwa lugha nyingine ndio mwanzo na mwisho wa kitabu kikubwa kama hiki.
          Hivyo katika kozi hii, na kama ilivyokwisha kuahinishwa malengo ya kozi hii, ni vyema kila mmoja wetu kuchukuwa wajibu wake, kusikiliza, kuuliza, kujadili, kufundisha na kufanya yote yatupasayo kufanya katika kipindi hiki ili kwa kupitia hapa tuwe mahili wa kusema ukweli mbele za watu juu ya imani yetu.

Mungu akubariki.


KITABU CHA MWANZO.

1.0 UTANGULIZI
1.1 Mazingira ya Kitabu cha Mwanzo.

          Kwa asili, Kitabu cha Mwanzo kilijulikana kwa   kiebrania “Bereshith” yaani mwanzoni au hapo mwanzo. Jina Mwanzo linatokana na neno Genesis lilitumika katika tafsiri ya Kiyunani, Septuagint (LXX).  Kwa Kiyunani   neno genesis limaana ya mwanzoni au _ya asili.
          Bereshith “Mwanzo” ni kitabu cha kwanza kati ya vitabu vitano vilivyojulikana ‘Vitabu vya Musa. Vitabu hivyo ni pamoja na Kutoka, Mambo ya Walawi, Hesabu na Kumbukumbu la Torati. Mara nyingine vitabu hivi hutambulishwa kwa jina la Pentatuki “tano”. Baadhi ya wanatheologia wanapendekeza kitabu cha Yoshua nacho kimo ndani ya vitabu hivyo.
          Kitabu cha Mwanzo kinabeba na kutunza historia ya dini ya kiyahudi, na kupenyezwa katika imani na tamaduni  mbalimbali duniani kwa namna ya kipekee. Hadithi zilizoandikwa katika kitabu hiki zinabomoa taratibu za kitamaduni na kujenga kitu kipya akilini na ndani ya maisha ya watu wengi leo duniani.
          Kwa ujumla sura hizi kumi na moja za mwanzo katika kitabu hiki zinahusika sana na habari za Mungu, Uumbaji, angako na Rehema ya Mungu.
          Jambo la msingi sana katika Kitabu cha Mwanzo 1 -11 inabeba ujumbe wa msingi wa imani kwa nyakati  zote na kwa watu wote. Kwamba kutokana na historia ya mtu mmoja watu wengi wakawepo. Lakini ikumbukwe kuwa Mungu ndiye asili ya uwepo wa vitu vyote. Mamlaka aliyonayo mtu, hutokana na Mungu.
          Kitabu cha Mwanzo kinaanza na kuonyesha picha Kubwa ya uumbaji wa dunia yote, na kisha taratibu    picha hiyo inafifishwa na kuzaliwa kwa taifa la Israel.  Lakini ijulikane kuwa Taifa la Israel lilikuwa ni gari tu la kurudisha picha ile ile ya kusudi la Mungu, kabla ya mwanadamu kuvunja uhusiano na Mungu (sur. 3)

1.2 Uandishi wa Kitabu.
          Wanazuoni wengi wa zama hizi wanakubaliana  kuwa Musa ndiye aliyeandika kitabu hiki kwa sehemu Kubwa kwa njia ya kuvuviwa na Roho wa Mungu. Hakuandika kwa njia ya imla: Mungu alisema, yeye anaandika maneno halisi toka kinywani mwa Mungu, aha! Alitumia lugha yake na uelewa wake wa kiimani  kuweka kumbukumbu za kimaandishi. Mbali na ushahidi wa wanazuoni, Biblia yenyewe inatoa ushuhuda tosha juu ya kazi hii: (Kut. 17:14; 24:4,7; 34:27; Hes. 33:1-2; Kumb. 31:9; Yos. 1:7-8; 8:32, 34; 22:5; Ezr. 6:18). Vile vile Agano Jipya linahakikisha kuwa Musa ndiye mwenye kuandika; (Math. 19:8; Marko 12:26; Yoh. 5:46-47; 7:19).
Kwa ujumla, inaaminika kuwa Musa ndiye aliyeandika vitabu hivyo, japo wapo watu wengine      walifanya uhakiki na kuongeza au kupunguza, au kupotea kwa sehemu zingine katika kitabu hiki. Kwa mfano Yoshua, yamkini ndiye aliyeandika juu ya kifo cha Musa (Kumb. 34).

1.3 Mitindo wa Uandishi
          Kitabu hiki kimeandikwa kwa mitindo ya aina mbalimbali kama vile: ushairi, unabii, na hadithi.
          Mtindo wa kiushairi au nyimbo unaonekana sana kujirudia rudia katika sura ya Kwanza ya kitabu hiki. Hasa kila baada ya kazi ya siku. Mtindo huu umefananishwa na liturgia au mtindo wa kiibada ‘Mungu akasema, na ikawa hivyo, ikawa asubuhi ikwa jioni siku .…’ na kwa kutumia ushairi mwandishi amefanikiwa kumwonyesha Mungu kuwa ni wapekee na wa kuheshimiwa ‘na tumfanye mtu kwa mfano na sura yetu ….’
          Hadithi, katika mtindo huu, ni wazi kuwa mwandishi anajaribu kuhabarisha kitu ambacho           kilifanyika miaka mingi iliyopita na kuleta kuwa chenye thamani kwa watu wa ulimwengu wake na hata       ulimwengu wa leo.[1] Sura ya pili, nne hadi ya kumi na moja ni mfululizo wa matukio jinsi yalivyotokea       kihistoria. Ujumbe wa unabii unachukua nafasi yake katika mtindo wa uandishi wa sura hizi, hususani juu ya ahadi za Mungu, sheria ya Mungu na baraka za Mungu kwa watu wake. Mungu kama kiini cha unabii, anatoa unabii juu ya yatakayomtukia mwanadamu               akimweshimu au kumdharau Mungu.
          Vile vile uigizaji, ukisoma sura ya tatu utaona  jukwaa pana lenye hadhira na fanani katika kujibizana. Japo unawezashindwa kumtambulisha mhusika mkuu na wale wadogo.
          Kitabu hiki kimeandikwa kwa ufundi mkubwa ili kwamba msomaji wa nyakati zote na kwa namna yoyote asichoke kusoma na kutafakari ujumbe wa kitabu hiki.
          Sasa basi baada ya kuangalia kwa ufupi juu ya mazingira ya kitabu, uandishi, na mtindo wa uandishi wa kitabu cha Mwanzo, tugeukie kuangalia mafundisho  yanayopatikana katika kila sura hizi kumi na moja.



2.0      SURA YA KWANZA HADI TATU
2.1 Muhtasari wa Sura ya Kwanza hadi ya Tatu.
          Sura za tatu za mwanzo kabisa za kitabu hiki,   zinajikita zaidi kuelezea hali ya awali ya Mungu katika kuumba ulimwengu na kila kilichomo, vinavyoonekana na visivyoonekana. Ni ukamilifu wa kazi takatifu ya   Mungu.[2]
          Pamoja na kuonyesha kazi aliyoifanya Mungu, bali pia mwandishi anatazamisha ulimwengu kuwa Mungu ndiye wa pekee tena mwenye nguvu nyingi kuliko kitu chochote juu mbinguni na chini duniani.
          Picha nyingine kuhusu sura hizi, ni mahusiano katika ya mwanadamu na kuitiisha dunia, mahusiano   yake kijamii na Mungu pia, udhaifu wa mwanadamu;  kutokumtii Mungu na kuongozwa na tamaa zake   mwenyewe na mwisho kujitenga na Mungu[3].

2.2 Mafafanuzi

          Kabla ya kuanza kufanya mafafanuzi ya sura hizi kama zilivyotajwa hapo juu, ni vyema sana kujuwa  namna ya kufanya ufafanuzi wa kifungu au neno kwa asili yake. Ili kutendea haki kifungu chochote cha maandiko haki yake, ni vyema kuhusisha maana yake ya asili kabla ya kuweka maana ya kiroho. Kwa hiyo    uchunguzi wa maana ya maneno na historia yake ni vya muhimu sana.
Katika kufafanua Kitabu cha Mwanzo na sehemu nyingine za Biblia. Kwa mfano neno ‘Mwanga’ linamaana ya nuru, au utukufu ung’ao. Maji kwa mfano, ni uhai,  lakini pia ni utakaso. Maana ya kwanza ndiyo ya asili na zile zinazofuata ni maana za kiroho zaidi.
          Aya 1. ‘hapo mwanzo’ Neno hili lilitumika kama jina la Kitabu, Ambato wayunani waliita genesis sawa na neno la kiingereza Genesis lenye maana ya hapo awali au kabla ya kuwapo na wakati wa kuwapo au kabla na wakati wa kuanzishwa kwa kitu.
          ‘Mungu’ ni roho isiyo na mwanzo wala mwisho, ni roho isiyotegemea kitu chochote ili iweze kuwepo. Hii inapelekea Mungu kuwepo daima. Kiebrania neno Mungu ni Elohim ambalo liko katika mfumo wa wingi. Lakini utajapo uumbaji Mungu anakuwa mmoja. Ukichunguza sana utagundua kuwa Mungu amefanya kazi hii kwa namna tofauti tofauti ya uwakilishi katika kazi. Kwanza ameonekana kuwa ni Mungu, kisha kama roho … (mtendaji).[4] Wakristo wanaibui theologia ya UTATU. Utatu ni nafsi tatu za Mungu mmoja. Mfano. Mungu anafikiri kisha anatamka, na mwisho anatenda. Lakini anabaki kuwa Mungu kweli (Yon. 1.1-11).
          Mungu ‘aliumba’, kwa kiebrania kuumba ni kufanya kitu pasipo kutumia kitu chochote ‘exnihilo’. Ni Mungu pekee ndiye awezaye kufanya kitu pasipo kitu kingine c.f 1,21,27. ‘Mbingu na nchi’ fungu hili la maneno mbingu na nchi linamaana ya kila kitu. Yaani hakuna ambacho Mungu hakukiumba aidha mbinguni au duniani. Hivyo Mwenye kupaswa kuabudiwa na kutukuzwa ni mmoja, ambaye yeye hakuumbwa na asili yake hakuna mwenye kuijua na wala hana mwisho.

 

         
          Aya 2, nayo nchi ilikuwa ‘ukiwa tena utupu’ Kuna hadithi zingine za uumbaji katika Mashariki ya mbali, Mesopotamia, ambazo zimetumia maneno hayo.   Kwamba Kuna mahusiano mkubwa kati ya uumbaji na Mungu, kwamba Maduk, ambaye alikuwa mungu mkuu juu ya miungu wengine alishinda nguvu za mungu  mwingine Tiamat aliyekuwa chanzo machafuko ‘chaos’.[5]
          Ushindi wa Maduk, kwa mujibu wa hadithi hizo ndio mwanzo wa kuumbwa kwa kila kitu. Uumbaji ulifanyakika kwa kutumia damu na mwili wa Tiamat na wengine Anu, anga na Ea, nchi.
          Turudi katika kifungu chetu, ‘ukiwa tena utupu’ isiyo na umbo, mpangilio, mamlaka na nguvu. Uwepo wa Mungu kama muumbaji unaiweka dunia katika mpango mzima kwa kadri atakavyo yeye.
‘Giza juu ya uso wa dunia’ kama tulivyosema hapo kwanza, kwamba dunia ilikuwa bado haina umbo, ilikuwa katika hali isiyo pangiliwa. ‘roho wa Mungu akatulia juu ya vilindi vya maji’. Roho wa Mungu, uwepo wa Mungu kabla ya vitu vyote kuwepo, uhai wa Mungu ndio unaoweka vitu katika utaratibu yakinifu (Kumb.32:11).[6]
          Aya 3-5, ‘siku ya kwanza: giza linaondolewa na Mwanza, sio kwa mwanga unaotokana na viumbo vya angani, hivyo viliumbwa baadaye c.f. 14-19. Mwanga  katika siku hii unagawa giza la machafuko, lisilokuwa  katika mpango. Mungu anaanza kuweka mpango katika uumbaji.[7]
          Kila siku ya uumbaji Mungu alianza kwa kusema ‘naiwe …’ ukamilifu wa kazi yake animaliza kwa kusema ‘na ikawa’[8] (3, 16, 21, 27). Hii inathibitisha uwezo wa neno la Mungu katika kuumba na kupangilia. Inaonyesha wazi nguvu na mamlaka ya Mungu juu ya uumbaji na vyote alivyoviumba, lakini pia inaonyesha lengo la   Mungu la uumbaji.
          ‘Ikawa asubuhi ikawa jioni’ kundi hili la maneno liafuata zaidi kalenda ya kidini wakati wa Agano la Kale, siku ilianza jioni (Law. 23:32). Mwandishi anatambulisha siku hizo kwa kutumia uzoefu wa mwanga. Kwamba kwa mwanga wa kwanza ndio siku na kupotea na kuanz tena basi siku zingine zinaendelea. Hivyo huanza linapochomoza na uisha linapokuchwa.

          Neno siku inaelezwa vyema katika aya ya tano. Moja kwa moja inamaana kwamba mchana               unatofautishwa na usiku wenye giza la asili, hivyo    inaunganisha siku nzima yaani masaa ishirini na nne. Kutokana na kifungu hiki, wanasayansi na wagudunzi wa kihistoria waatathmini kuwa Kitabu cha Mwanzo katika sura hizi za mwanzo ni fikra tu za kidini ili kujenga imani thabiti kwa waumini wasomao kitabu hiki.


 

Katika makundi, jadili mambo muhimu
 aliyoyafanya Mungu katika siku ya kwanza.

            Siku ya pili: aya ya sita hadi nane. ‘kuteganisha’ neno hili limetumika sana katika uumbaji kwa siku tano. Mungu ametenganisha giza na mwanga, usiku na   mchana, mbingu na nchi, maji ya juu na ya chini, nchi kavu na bahari, vile vile ametenganisha wanyama wafugwao na waporini. Mungu hutumia kitu cha kwanza kufanya kitu kinachofuata. Haimaanishi hakuna stadi yoyote aliyoitumia Mungu katika uumbaji, Mungu anabaki kuwa Mungu na vile anavyoviweka kwa utaratibu wake vinakuwepo.


 

Katika makundi, jadili mambo muhimu
 aliyoyafanya Mungu katika siku ya pili.
           
          Siku ya tatu, aya tisa hadi kumi na tatu. Aya 10, Mungu akaita, Kutoa jina kwa kitu hasa katika          utamaduni wa kiyahudi ni kuonyesha uwezo alionao mtaja jina dhidi ya kitajwacho. Cf. 2 Fal. 23:34) (tuaingalia zaidi sura ya 2:19.
          Aya 11: ‘Kwa aina zao’ Mungu aliweka mpaka wa kudumu kati ya wanyama na mahusiano katika       kuendeleza mahusiano. Kifungu hiki kinatofautiana na habari za kimabadiliko ya maumbile ‘evolution’ kwamba uwepo wa kuishi kwa viumbe na mwonekano wao waleo ni zao la mabadiliko yaliyochukua miaka milioni zaidi ya 20. kwa mfano, mwanadamu amepitia hatua tano hadi kufikia hali aliyonayo leo kimaumbile na akili. Vile vile na wanyama wengine pia.
          Utofauti wa kifamilia unatokana na genetiki asili ya kundi fulani la wanyama. Hakuna wanyama           wanaoshiriki genekia moja hata kama wanaukaribu wa kufanana. Mungu ni mwanasayansi wa kwanza ya kibaiolojia na sayansi zinginezo.
KATIKA MAKUNDI, JADILI
mambo muhimu aliyoyafanya Mungu katika
siku ya tatu.
         
Siku ya nne: Aya 14-19, ‘Mianga’ mwanga wa siku ya kwanza unatofauti na mianga hii. Mianga hii inatokana na viumbo vilivyoumbwa na Mungu ili kuonyesha majira ya mwaka, usiku na mchana, siku za kuabudu alama za hukumu (Math. 24:29) na kuwezesha mimea kukuwa.


 

Katika makundi, Jadili, Umuhimu wa jua
katika ibada na  maisha ya kila siku,   
faida na hasara zinazotokana na jua.

          Siku ya tano. Aya 20 hadi 23, Mungu anaumba kila kitu; tangu viumbe viendavyo angani, wanyama waishio majini, na viumbe wengine wengi kwa namna zao. Neno ‘Kuumba’ mst. 21, lionyesha ushiriki wa  Mungu katika kazi ya kuvifanya vyote kuwepo.
          Baraka ya kwanza inatolewa kwa kundi hili la viumbe. Mungu anatoa baraka hii kwa viumbe hao ili waishirikishe baraka hiyo ya uumbaji kwa viumbe wenzao na kwa vizazi vyao vyote. Mungu aliwaumba, vile vile wao waendeleze nguvu ya uumbaji waliyopewa na Mungu. Tutaangalia kwa kina kwenye mafundisho.



“Mungu ni asili na mwanamazingira”.
Jadili usemi huo ukilinganisha na hali ya mazingira sasa. Toa maoni
yako nini kifanyike kuboresha hali ya mazingira.

Siku ya sita, aya 24 hadi 31: Katika aya hizi, uumbaji umefanyika katika makundi makuu mawili; la kwanza ni uumbaji wa viumbe vye uwenyeji katika nchi kavu ambao wamegawanyika katika sehemu kuu tatu; wanyama wa porini, wanyama wa kufugwa na wanyama wenye damu baridi, na wengine wote waishio juu ya sura ya dunia. Japo kusudi ni uumbaji wa pili ambao ndio kilele cha uumbaji wote. Uumbaji huu ni wa mtu, ‘adam’.
          Nini kinachomtofautisha mwanadamu na wanyama wengine?
          La kwanza kabisa lugha ya uumbaji, toka katika kaamuru tu na kuhusika katika nafsi, ‘na tumfanye mtu ...’ Swali jingine, ni kwa nini nafsi ya kwanza wingi inatokea hapa; ‘tumfanye’? Tutaangalia katika sehemu ya mafundisho muhimu.
          Sababu ya pili ya kutofautiana na wanyama wengine ni ‘mfano na sura yetu’ mfano mara nyingi   imemaanisha kuwa ni sanamu yenye kuwakilisha kitu Fulani. Au inamaana ya nakala ya kitu Fulani chenye mfanano na kile cha awali.
          Mwanadamu anatofautishwa na wananyama wengine kwa kuwa anauwezo wa kufikiri, kushirikiana, kuamua, kuweka kumbukumbu na kujua mema na mabaya. Hivyo ukaribu wa mwanadamu mbele za Mungu unamfanya kuwa kiumbe cha pekee kati ya viumbe.
Aya 27, ‘akamuumba mtu’ mwandishi hakuonyesha mtu aliyeumbwa ni wa jinsia gani. Tofauti za kijinsia ni mpango wa Mungu wa uzao na ushirikiano kwa ajili ya kufanya dunia kuwa sehemu muhimu ya kuishi kwa viumbe alivyoviumba. Katika siku hii Mungu alimuumba mtu mume na mke kwa kusudi lile lile la   kutegemeana.
          Aya 29-30, kwa mpango wa Mungu wa kumuumba mwanadamu ulikuwa mtu huyu awe ni mwenye kula mazao yatokanayo na mimea na matunda. Wanyama wengine nao vile vile wapate chakula chao kutoka na mimea kama nyasi na mti pia.

Katika siku hii ya sita, Kwa nini Mungu anatoa baraka? Nini nafasi ya Mwamke na mwanamume katika uumbaji wa Mungu?


SURA YA PILI
2:1-24

          Sura ya pili ya kitabu cha Mwanzo inaelezea ukamilifu wa kazi ya Mungu ya uumbaji. Kwa maneno mengine, sura hii inarejea kwa kufafanua kile kilichotokea katika siku ya sita (sura ya kwanza). Hakuna kilichofanyika cha kiumbaji katika sura hii. Mara nyingi tumesema kuwa mwanamke aliumbwa baada ya juma la uumbaji, sio kweli. Mungu aliwaumba wote siku ile ile alipomuumba Adamu.

          Aya 1, ‘mbingu na nchi zikakamilika’. Kila kitu alichopanga Mungu kiwepo kwa makusudi ya uumbaji kilikuwepo. Baada ya kazi zote aya 2 ‘akapumzika’. Kupumzika ni kufurahia kazi uliyofanyika. Mungu hapumziki, kila wakati yuko kazini. ‘siku ya saba’ kwa Kiebrania Sabbath, ilikuwa siku baada ya siku saba, lakini baadaye ilifanywa kuwa rasmi tofauti na siku nyingine. Siku hii ilitengwa kwa ajili ya ibada tu.
          Kusudi ya siku hii ni kufanya mahusiano na watu wengine, kuwapenda, kuwahudumia wahitaji,           kuupumzisha mwili na akili kwa mambo makubwa na mazito yanayochukua muda mrefu. Mungu hakupumzika, alifurahia uumbaji. Hii ndiyo maana ya sabato “kupumzika” ni siku ya furaha. Paulo anasema ‘furahini katika Bwana tena nasema furahini.’ Furaha ya kweli inaleta pumziko la ndani, na sio la mwili. Furaha hiyo itakamilika pale tu, Yesu Kristo atabadili maisha haya.
          Aya 4-25, ni nyongeza mpya katika sura ya kwanza. Ukisoma katika biblia ya Kiebrania utaona     tofauti ya kihistoria na lugha iliyotumika kumtambulisha Mungu (documentary hypothesis: JDEP); sura ya kwanza Mungu anaitwa Elohim, sura ya pili YHWH lenye maana ya niko na mkombozi.
          Aya 5: mimea inayotajwa hapa ni ile yenye kulimwa au kupandwa haikumea hadi baada ya kuumbwa kwa mwanadamu, kwa vile ili hitaji uangalizi wa karibu.

Sura ya Pili, inaelezea uumbaji baada ya uumbaji wa kwanza. Jadili.

          Aya 7: Mtu anaumbwa kutoka katika udongo. Maana ya mtu ni udongo (1Kor. 15:47), kitu ambacho hakina ukamilifu, chenye kutegemea kitu kingine. Lakini maisha yake yanatokana na pumzi ya Mungu. Wanyama nao wanashiriki katika pumzi hii, mtu anaongeza sifa zaidi kwa kufanana na Mungu.
          Aya 9-12 ‘mti wa uzima na mti wa ujuzi wa wema na mabaya’ miti hiyo ilipewa umuhimu mkubwa na Mungu. Vile vile Mungu aliweka katika nchi kila samani kwa ajili ya mwanadamu. Pia Mungu alimpa ruhusa na zuio kutenda au kutokutenda mambo kadha wa kadha.
          Mwanadamu aliruhusiwa kula kwa uhuru kila kitu katika bustani alichoamriwa kula kwamba vimebarikiwa na Mungu kama matunda na mboga mboga. Usalama wa chakula utakuwepo daima. Usalama wa chakula ni  upatikanaji wa chakula bora, cha kutosha, kwa watu wote na kwa wakati wote. Hivyo lilikuwa kusudi la Mungu, mwanadamu asipungukiwe chakula bora.

Vile vile aliruhusiwa kufanyakazi kwa niaba ya Mungu ili kuweka vitu vyote katika mpangilio sahili. Kulima na kutunza mazingira zilikuwa sehemu za kazi aliyopewa mwanadamu.
          Pamoja na kuruhusiwa kuwa huru kufanya kila kitu bustani kwa namna ya mapenzi yake mwenyewe, alizuiliwa kufanya mambo kadha; asile na akila atakufa. Wajibu wa mwanadamu ulikuwa kumtii na kumtegemea Mungu pekee, kutenda kinyume na maagizo ya Mungu kulilenga kuondoa baraka. Baraka ambayo ni chimbuko la furaha na amani.
          Aya 15-20; Mungu anampa Adamu wajibu wa kufanya. Moja, kazi ya kulima bustani, pili kuangalia na kuitunza, tatu kula matunda yake isipokuwa mti wa ujuzi wa mema na mabaya na nne kumiliki wanyama wote.
          Aya 18 ‘msaidizi wa kufanana naye’ mwenza wake, ubavu maana yeke ni upande, au sehemu yeke yenye kufanana au yenye asili moja. Hivyo mke  anatokana na asili ile ile ya uumbaji.
          Aya 24 ‘mwili mmoja’ ni kanuni ya mahusiano ya kudumu. Kifungu hiki kinaonyesha mahusiano kati ya mume na mke, upendo ndio unaosababisha kuwaacha wazazi. Kuwa mwili mmoja ni sawa na kanuni hii. Kuondoka ni sawa na moja, kuambatana sawa na mbili na, mwili mmoja ni sawa na tatu.
‘Uchi’ katika mstari wa ishirini na tano, unahusika na mazingira ya mahusiano katika ndoa na sio kutokuwa na nguo. Faragha na heshima ya ndoa ni kuutunza uchi. Uchi  usipotunzwa huleta haibu. Hakuna mpaka katika mahusiano baina ya mume na mke. Huo ndio ulikuwa mpango wa Mungu kwetu sote.
          Mambo muhimu ambayo Mungu anaagiza mume na mke kutekeleza;
          Moja ni jamii, “si vyema mwanamume kuwa pekee   yake ….” ili aweze kuijaza dunia alimpa Eva. Na      akaanzisha taasisi ya ndoa ili kuendeleza kazi ya  uumbaji. Sifa ya taasisi hii ni pamoja na kumpenda    Mungu, na kumpenda jirani bila kujali rangi, utaifa, ukabila, elimu, cheo nk.
          Kuupangilia uumbaji, Mungu aliwaamuru kukunza na kuendeleza kazi yake takatifu ya uumbaji. Kama Mungu alivyoweza kuumba, kugawanya, kukusanya, nk., vivyo hivyo mume na mke wanatakiwa kusimamia kazi hiyo kwa utiifu mkubwa. Kuwatawala wanyama pasipo uharibifu, na kulima kwa kanuni zote za utunzaji wa ardhi kwa ajili ya kizazi kijacho.

Tafakari juu ya Maswali yafuatayo:                                       
·    Unajifunza nini juu ya mti wa ujuzi wa mema na
   mabaya?
·    Ni nini maana ya msaidizi.
·    Taja sifa za msaidizi


MWANZO 3.1-24

          Baada ya kuangalia mafafanuzi ya sura mbili za mwanzo kabisa za kitabu hiki, sasa tuangalie sura ya  tatu. Sura ya tatu inaujumbe tofauti sana na sura zilizotangulia. Kwani katika sura hii tutaangalia jinsi maisha ya mwanadamu na mahusiano yake kwa Mungu wake yalivyo badilika na kuleta utengano mkubwa. Makundi muhimu katika sura hii ni Mungu, wanadamu na nyoka.
          Tunaambiwa nyoka alikuwa mwelevu zaidi ya wanyama wote wamwitu walioumbwa na Mungu. Kuna mijadala mingi sana ya kumwelezea nyoka kuwa alikuwa nani au nini katika hadithi hii.
          Wapo wanaosema kuwa shetani alikuwa ni mwongo, wazo hili linalinganishwa na hali ya shetani katika kumjaribu Yesu kwa njia ya upoteshaji wa ukweli wa neno la Mungu.
          Wengine wanaamini kuwa uwezo wa akili kudadisi, shetani anapatikana katika mawazo ya Eva na kumtamanisha katika kutamani ufahamu   zaidi.
Wapo wasemao ni mapepo kwamba shetani ni  Pepo mchafu, asiyemtii Mungu na watu, ndiye mungu wa kuzimu chanzo cha kifo. Vile vile alionekana kama mnyama kweli mwenye kuweza kuzungumza.
                  

Kwa ajili ya umuhimu wa sura hii katika maisha yetu, njia ya kujifunzia itajikita sana katika maswali na majibu. Ili kila mmoja wetu aweze kushiriki vizuri na kuelewa vyema ujumbe wa sura hii.
Shetani anabadili maagizo ya Mungu, Eva naye anakubaliana na shetani vile vile. Dhambi ni nguvu za kimapepo zilizomo ndani ya mtu. Kwa maneno mengine, dhambi ni hali ya kuwa na chuki kwa Mungu ambapo hali ya kupingana na kuzozana kunaibuka dhidi ya utawala na mamlaka ya Mungu.
Kukataa huruma ya Mungu, Pamoja na kwamba Mungu anaonyesha huruma kwa Adamu na Hawa bado roho ya kujiinua imewajaa na kukataa kabisa kumsikiliza Mungu. Swali la Mungu linalenga kuwarudi ili kwamba wakubali mamlaka ya Mungu kwa upya.
Macho yao yalifunguka, wakagundua mambo mapya ambayo hawakuwahi kushiriki na kutenda. Sasa waweza kujificha, wanajitengenezea mavazi, wanaanza kujitegemea kuliko kumtegemea Mungu, wanavunja   ushirika na Mungu na maisha yao yanakuwa tena si ya shirika, kila mmoja anamwona mwenza wake ndiye   chanzo cha tatizo.
Aya ya 8 hadi 24 inaelezea matokeo ya kuvunja kanuni na sheria za Mungu. Aya hizi zinaweza kugawika katika sehemu kuu nne; hatia, mashitaka, laana na mwisho ni utumwani.
Hofu na hatia (8-11), Picha ya ‘kutembe’, kwamba Mungu anawatembelea wanadamu katika bustani ya Eden. Picha hii inaonyesha ushirika aliokuwa nao Mungu kwa watu wake. Tamaa ya Adam na Hawa kutaka kufanana na Mungu ndio iliyosababisha mahusiano haya kuvunjika. Kutembea ni sawa na uwepo wa Mungu  wakati wote. Cha kushangaza, Adam na Hawa walijificha wakifikiri kuwa Mungu hawezi kuwaona. Lakini Mungu ni roho yenye kuwepo mahali pote kwa wakati wote.
‘Uko wapi?’, sio kwamba Mungu hawezi kuona    walipo Adam na Hawa, lakini inamaana ya; Mungu      lazima alijuwa wako wapi, katika mwili na kiroho, alitaka wajitambue na kuelewa hali ya mahusiano yao na Mungu kwa wakati huo. Mwanadamu kwa hakika hakujua ni kwa jinsi gani Mungu atavyolichukulia tatizo la kutomtii. ‘hakika siku utakapo Kula utakufa’. Utakuwa umevunja mahusiano na Mungu.
          Mashtaka, mwanadamu hakuweza kuchukua wajibu wake hasa kwa kosa alilotenda. ‘mwanamke uliyenipa…’ huyu ndiye aliyependezwa naye na kumtaja kama mama wa wanadamu wote. Hapa anamkana si wake tena, bali ni wa Mungu. Dhambi hukuwa pole pole kwa kuanza na kutokuikubali japo nafsi inajua kabisa kuwa imetendeka.

Laana (14-19), laana ya kwanza ilikuwa ni adhabu kwa shetani, ambaye anaonyeshwa kama mvamizi hivyo atembea kwa tumbo, atakula mavumbi na atamgonga mwanadamu kisigino, naye atapondwa kichwa. Kuna maana mbili kubwa hapa: ya kwanza ni shetani atakuwa si wa milele, katika kutenda kwake atamtegemea Mungu kwa kuwa yeye, shetani hana mamlaka na uweza juu ya ulimwengu na mbinguni. Pili, kutakuwepo na uadui katika ya mamlaka ya shetani na Yale ya Mungu. Uzao wa  shetani na mapepo na uovu wote, uzao wa mwanamke ni Yesu Kristo na nguvu zote za Mungu mbinguni na duniani. Au waweza kusema ujumbe huu ulikuwa ni unabii wa kuja kwa Kristo Yesu kwa ajili ya kukamilisha mpango wa Mungu wa kumkomboa mwanadamu.
          Laana ya pili ni juu ya mwanamke, tokeo la kutotii kwake ni kuongezewa utungu wa kuzaa. Hivyo hali ile ya kuwa na sifa ya mama na mke iliathiriwa na ikaingia   katika laana, hakuna furaha.
          Mahusiano kati ya Hawa na muge (MST.17) utakuwa tena si mzuri kwa sababu ya kujitenga na   Mungu, mume anaanza kumtawala mwanamke na mwanamke anauwa mnyonge na mwenye kubebeshwa mzigo mkubwa wa majukumu. Utungu alionao mwanamke ni ongezeko la kazi za uzalishaji mali kwa ajili ya familia yake, jamaa ya mume wake na taifa kwa ujumla. Mwanamume anakuwa mwenye Kula kwa starehe asicho  kuandaa.
Maswali:
Shetani anatumia njia gani kumdanganya Hawa?
Hawa anafanya kosa gani?
Hatia ya Adamu nini?
Laana ni nini (je, leo kuna laana?).

          Adamu alikubaliana na mkewe kula tunda la mti uliokatazwa. Alisikiliza maneno ya mkewe. Pia Adam   alikataa kosa lake pale alipoulizwa na Mungu, “kwa nini umekula ….?”
          Laana kwa mwanamume ikawa tofauti, atafanya kazi kwa nguvu na kula chakula chake kwa jasho. Maisha na kifo vinaanza kukinzana, bila kufanyakazi utakufa. Wakati huo ardhi nayo haitazalisha chakula kwa kawaida yake, kwani ardhi itachakaa na kusababisha uzalishaji duni. Hivyo kazi itakuwa ni siku zote na ya  kuchosha ili kukidhi haja ya maisha.
          Utarudi mavumbini (mst . 19), Adam na Hawa  waliumbwa kwa mfano wa Mungu, sura hiyo sasa imebadilika na kurudi katika hali yake ya kawaida yenye uharibifu. Hataishi tena milele, atakuwa tegemezi, asiyenamaamuzi mazito ya kujitegemea.
         
Jambo jingine la Muhimu ni kupelekwa utumwani. Hapo kwanza Adam alikubali kuwa mwanamke ndiye mama wa maisha ‘mama wa wote’. Hii ilikuwa karama pekee ambayo mwanamke alipewa na Mungu na wanawake wote ili kukuza na kuendeleza jamii. Hata baada ya tumaini la kuishi milele, bado mwanamke alitengwa kwa ajili ya ukombozi wa ulimwengu “kizazi chako kitamponda kichwa” (3.15).
          Mpango wa Mungu wa ukombozi alianza mara tu baada ya anguko la mwanadamu. Utekelezwaji wake unaonekana dhahiri kwa kupitia Sara (21.1-2), Hana (1 Sam. 1.20), Elizabeti (Luka 1.13) na Mariam (Math. 1.18). Nafasi ya mwanamke katika ukombozi na upatanisho katika Mungu na watu umepewa nafasi ya kipekee katika Biblia. Japo katika ulimwengu wanyama twaweza kusema kwa nguvu kuwa mwanamke ni chombo dhaifu.
          Picha katika mstari wa 21 ni kama igizo linalomjumuisha Mungu. Adam na mkewe walishindwa kufunika aibu ya uovu wao. Mungu aliwakubali jinsi walivyo kama watu wadhaifu sana. Lakini ilimgharimu sana katika uumbaji ili kuwafunika aibu hiyo. Aibu hiyo ilifunikwa kwa ngozi ya mnyama asiye na hatia na kufanyika kuwa sadaka ya kutotii.
          Huu ni unabii wa mafundisho ya upatanisho uliofanywa na Musa, na kisha kukamilishwa na kifo cha Yesu msalabani. Kusudi kubwa la fungu hili ni kututazamisha kuwa asili ya Mungu ni kutokuangalia  udhaifu wetu, bali gharama ya kuondoa udhaifu huo kwa kifo cha mnyama asiye ana hatia. Lakini pamoja na udhaifu unaomgharimu Mungu kwa kiasi kikubwa, bado anatukaribisha kuwa na ushirika pamoja naye.
          Kwa yeyote amwondoaye Mungu, nafasi zao zitaondolewa. Watapoteza haki ya kumfikia Mungu kama Mungu na rafiki yao katika kufurahia maisha na mali za dunia hii. Mwanamke na mwamume walifukuzwa katika Bustani ya Edeni ili wasifurahie tena raha ya Mungu. Kwa kula mti waliokatazwa ilitosha kabisa kuingia katika  kujua mema na mabaya. Hakuna atakaye weza kukwepa utumwa huo isipokuwa amekubali kukaa Edeni na kufuata kanuni zote kama zilivyo.
          Biblia inahabarisha ni kwa njinsi gani Mungu alivyotoa njia ya kuishi Edeni na kuendeleza mahusiano. Lakini nguvu ya uharibifu ilitosha kuvunja kila kitu. Je, kunaweza kuwepo na vyanzo vingine vya hekima ya kuishi? habari hii inasisitiza kuwa hakuna. Hekima ni Mungu pekee. Vyanzo vingine ni uongo na upotevu.
          Tunahitaji hofu sio uovu, kwa sababu Mungu   hajaficha mamlaka yake kwa yeyote. Yeye ndiye    mwandishi na mhukumu wa maisha. Imani ndiyo njia pekee iletwayo na Injili kuwa katika Kristo Yesu twaweza Kumba Mungu nafasi yake ya Utukufu, nguvu na heshima. Hakuna njia nyingine ya kuurudia mti wa    uzima.

MASWALI YA KUTAFAKARI.
  1. Ni kwa namna gani hadithi ya uumbaji katika Mwanzo 2 na 3 zinatofautiana na Mwanzo 1.
  2. Ni ndoa ya namna gani imeelezwa katika Mwanzo 2.26 (linganisha  na sura ya 10.6,9)? Kwa nini ndoa nyingi za Kikristo zinavunjika?
  3. Jinsi gani wakristo wanafafanua ‘tupu’ na ‘uchi’? Unafikiri wakristo wanatumia vipi utupu katika:
          A) Utengenezaji wa sinema au dansi
          B) Matangazo mbalimbali.
          C) Makusanyiko ya wazi.
          D) Nyumbani na katika familia.
     4. “Anaye atakutawala” (3.16). Je, wazo hili  
          linabariki mume kuwa juu ya mke kuanzia ngazi 
          ya kijamii na kanisa pia? Je, kwa kuwa 
          kimetokana na laana, twakitumia namna gani?





MWANZO 4-5
4.1-7: Ustaarabu, familia na uhusiano.
         
Baada ya kuangalia sura tatu za mwanzo katika kitabu hiki chenye historia kubwa ya imani yetu, napenda kuwakumbusha mambo muhimu sana tuliyojadili.
          Kwanza tumeona nafasi ya Mungu katika kifanya dunia na kila viijavyo kuwepo katika utaratibu wake bila ya kuathiri uwepo wa viumbe wengine. Vile vile tumeona mahusiano ya awali ya Mungu na viumbe wake hususani mwanadamu. Mungu alimkabidhi ulimwengu kuutiisha na kuutumia na kuendeleza.
          Pili, tulipokuwa tunajadili sura ya pili tumeangalia umuhimu wa mwanadamu katika mpango wa Mungu, lakini pia, tumejadili juu ya mambo makubwa manne: katazo la mti wa uzima na mabaya, upweke, mahusiano kati ya mtu na wananyama wengine na kisha na  mkewe. Yaani kusudi la Mungu la mtu mume na mke (ndoa).
          Ni vyema kutambua ya kwamba, Kitabu cha Mwanzo kimeweka mambo machache kwa ajili ya kuufaa wokovu tu. (Yoh. 21.25).
          Sura hizi nne hadi tano, zinaleta mwendelezo wa maisha ya mwanadamu na jinsi walivyozidi kwenda mbali na Mungu wao. Umbali huo ulisababishwa; ama ustaarabu au roho ya kutotii kama ilivyotokea kwa Adam na Hawa. Kwa mfano kaini na nduguye Abel, mnara wa Babeli, maisha ya vizazi baada ya Adam nk.
          Vyema kuanza na maisha ya kawaida ambayo
Adamu hakuwahi kuyaisha hadi alipofukuzwa Edeni.   Katika sura ya nne, mstari wa kwanza ‘akamjua’ inaweza kuwa na maana zaidi ya mbili katika biblia. Hapa ni kumjua mkewe. Kwa kiebrania kujua linamaana ya tendo la ndoa. Katika sura ya pili tulisema kuwa ndoa ni watu wawili: mume na mke, kisha mwili mmoja ni mtoto au watoto. Hivyo kujua ni kujamiana kati ya mume na mke ili kupata mtoto. Hawa akamzaa Kaini. Baadaye   tena akamzaa Abel.
          Ukweli kuhusu baraka za Mungu zinaanza kudhihirika kwa wanandoa hao. Kuongezeka ilikuwa   ahadi ya msingi ya Mungu si kwa mwanadamu hata kwa wanyama. Hata baada ya kutenda dhambi, Mungu hakuibatilishi. Ilisimama pale pale.
          Mgawanyo wa kazi unaanza mapema kabisa kama sehemu ya wajibu wa kila mwanafamilia. Mgawanyo huo ni picha halisi ya tamko la Mungu “mtakula kwa jasho.” Kazi ni wajibu wa kila mmoja, hakuna kukwepa wajibu huu, lazima kufanya kazi. Asiyefanya kazi asile.
         
Jamii ya ufugaji na ile ya wakulima huwa na migongano ya mara kwa mara japo jamii hizi           hutegemeana sana katika maisha. Mjadala kuhusu maeneo ya ufugaji unapewa nafasi kubwa zaidi ya     majadala juu ya maeneo ya kilimo. Hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa familia ya Adam na Hawa.
Abel alipokuwa mfugaji na Kaini alikuwa mkulima, jamii ikaanza kuchukua sura. Katika uwajibikaji kikazi, hakuna kazi iliyobora zaidi ya nyingine. Kazi zote ni sawa. Isipokuwa thamani ya kazi itatokana na mwenye kuifanya kazi hiyo. Kaini alishindwa kuifanya kazi yake kuwa ya thamani mbele za Mungu, lakini Abel aliithamini kazi yake na kupandisha katika kilele cha ubora mbele za Mungu.
          Ustaarabu wowote, huja kwa kugawanywa kwa matabaka ya fani. Fani hizo zikiingia katika ushindani ndipo msuguano wa kimaslahi uibuka. Japo wataalamu wa maendeleo ya jamii husema msuguano ndio chachu ya maendeleo.
          Jina Abel linamaana ya ‘mavumbi’au ‘pumuzi’ ambayo inalenga kuonyesha ufupi wa maisha ya        mwanadamu; baraka, kazi, taabu na kisha mauti.
          Sadaka ilikuwa jambo la kawaida katika dini mbalimbali za mashariki ya kati. Hii ilikuwa inaoanishwa na hali yao kiuchumi, matabaka ya umilikaji mali na  uzalishaji pia. Hasa sadaka ilitokana na mambo makuu mawili: vitokavyo na tumbo, ardhi, anga na maji. Tangu mwanzo, watu walitambua kuwategemea nguvu za miungu kwa ajili ya kuendesha maisha yao. Sadaka ya Abel na Kaini ni ushahidi wa utegemezi huo wa kiimani.

Mungu anapokea kwa namna tofauti sadaka ya Kaini na Abel. Abel alitoa sadaka bora na sadaka ya Kaini haikuwa bora. Kutokana na ufafanuzi wa Matengenezo, Abel alichaguliwa na Mungu, Kaini alikataliwa. Hoja ya mwandishi haikuwa ni namna gani Kaini alijua kwamba sadaka yake imekataliwa, ila ni kwa jinsi gani Kaini ilivyohusika na kukataliwa kwa sadaka yake.
          Maisha nje ya Edeni yanakumbwa na changamoto nyingi, kutenda kwa haki, vita, mauaji, wivu na mengine kama hayo. Kinachojalisha hapa ni kwa namna gani mtu hukabiliana na nguvu zenye msukumo hasi au chanya. Kaini alivutwa na msukumo hasi.
          Kaini anamjia juu Mungu kwa kukuikubali sadaka ya mdogo wake. Kaini hakuwa na furaha tena dhidi ya ndugu yake. Kaini akakata mawasiliano naye, hakutaka kumtazama hata usoni. Hii inafanywa na watu wengi hasa wanaposhindwa kufikia malengo fulani katika maisha, na hasa wanapoona wengine wakifanikisha.  Watu hao huwa na wivu na hasira sana.
          Wenda Kaini alikuwa na sababu ya kuwa mwenye hasira na kukasirika ni sehemu ya kumkamilisha mtu. Lakini alishindwa kuijuia hasira na wivu wake hata kusababisha kuharibu mahusiano ya kifamilia. Kusudi la Mungu kuunda familia ni kuwa na umoja unaoweza kutuleta kwa Mungu.

Baada ya Adam kutenda dhambi, Mungu alimpa nafasi kutambua tendo lake, kutubu na kuanza upya. Mstari wa sita, Mungu anapa nafasi Kaini  kutambua tendo lake ovu. Swali, ‘kwa nini una hasira’ inamkaribisha Kaini kujitambua nini kinachotendeka ndani, inaweza kuwa ni namna ya ushauri. Matatizo mengi ya kihisia hutatuliwa kwa mazungumzo. Huu ni mpango wa Mungu wa kutokutaka kumpeteza hata mmoja. Mungu anamwonya Kaini kuiweza hasira yake na sivyo azingwa na shetani. Ulikuwa ni uamuzi wake kuacha au kutenda.

Mwanzo 4.8-16:
Kifo na matokeo yake kwa mtu binafsi na jamii
          Kila dhambi inakuwa na mpango kazi na hutekelezwa kwa umakini mkubwa (mst. 8). Abel     hakujua mpango huo, endapo angelijua naamini asingeliambatana naye. Kaini kama Baba yake,         anaulizwa na Mungu ndugu yako yuko wapi? Jibu la kaini linakuwa “sijui, mimi si mlinzi wa ndugu yangu.’ Ni vigumu sana kwa mtu kukubali ukweli hata kama ni dhahiri, mara nyingi tunasingizia tu. Kaini yeye anaanzisha vurugu dhidi ya Mungu. Kaini alitakiwa kumlaumu Mungu na wala sio ndugu yake. Zaidi alitakiwa kuchukua wajibu wake.
          Mst. 10, Kaini alidhania kuwa kwa kumuuwa nduguye ndio ulikuwa mwisho wake, Abel. Katika aya hii Tunasikia sauti ya Abel ikilimlilia Mungu. Kaini alitatua tatizo kwa kuzalisha tatizo, tatizo haliishi litaendelea kumea. Hii ni sawa kwamba Kaini hauwa salama, kwani bado kifo kipo mbele yake na kitamkabiri kwa namna yoyote: magonjwa, msungo wa mawazo, n.k. Mungu anasema wazi kuwa hasira na wivu wa namna hiyo hauzikwi kaburini.
          Hata ardhi ambayo Kaini anaitegemea kwa uzalisha wa chakula chake, sasa inamkataa kwa       kumzalishia chakula kichache baada ya kufanyakazi nzito. Dhambi mara zote ulinganishwa kati ya uchumi na muhemuko.
          Laana kwa Kaini zinaweza kugawanywa katika sehemu kuu mbili: ya kwanza, uzalishaji na kufanikiwa kiuchumi itakuwa kwa maumivu zaidi (mst. 12), ya pili, ataishi kwa kuweka miiko na kanuni kwa jamii yake mwenyewe.
         
Pamoja na kumlaani, Mungu bado alikuwa bega kwa bega na Kaini. Alimwekea alama, sio chale za moto kama ‘tatoo’ ila ni ulinzi wa kimungu dhidi ya maadui, sawa ambavyo Mungu alifanya kwa Adamu, aliwatengenezea nguo kwa ngozi na kuwafunika. Nodi haukuwa mji wa kijiografia, ilimaanisha jinsi ambavyo Kaini ataangaika huku na kule katika ulimwengu kama wazazi wake walivyofukuzwa Edeni na kuelekea mashariki ya Edeni  yaani kusikojulikana. Yote hayo    yanaonyesha utengano wa mwanadamu na Mungu wake.
         

Mwanzo 4.17-5.26
WATU NA KUSUDI LA MUNGU
         
          Sura hii ya nne inaonyesha vizazi viwili muhimu sana katika historia ya imani ya kiyahudi. Uzao wa Kaini na ule wa Sethi. Uzao huo unaoonyesha kusudi la Mungu kwa jamii.
          Kwanza, kutokana na historia za wa kanani juu ya uzao wa Kaini, kwamba unaonishwa na ukuaji wa miji, kunama hama, mambo ya muziki na desturi za jamii ya mwanadamu ziliibuka baada ya dhambi ya Kaini. Wazo ni kwamba, nje ya Edeni, jamii, ugunduzi na desturi zinashika kasi. Lakini msingi wa utamaduni wa Mungu unabaki pale pale, kuwa ujenzi na usimamiaji wa jamii unadumishwa.

Familia ya Kaini
          Sehemu ya kwanza ya uzao wa Kaini (4.17-18) inajumuisha vizazi saba: Adam, Kaini, Enoko, Irad, Mhujael, Methusela, and Lameki. Na sehemu ya pili (4.19-24) inataja vizazi na mtindo wa maisha walioishi. Kwa mfano, maisha ya kuhama hama yalikuwa ni sehemu ya mtindo wa kuishi kwa Israel (Kumb. 26.5-9).
          Majina ya kizazi cha wakaini kinaonyesha asili ya waebrania na mwanzo wa kumiliki na kujenga jamii yanye nguvu. Kila jina linamaana yake. Irad sawa na Eriud – mji mkongwe wa Mesopotamia. Mehujael – Mungu atoaye uhai. Methusela - mtu wa Mungu aliye chini duniani. Lameki maana yake Mungu wa anga au kundi la makuhani. N.k.
          Ugunduzi wa chuma na shaba na matumizi yake ni ishara kuwa jamii hizi zilikuwa zinakuwa kiteknologia, kijamii, na kiuchumi pia. Madini ni mali ya Mungu, ametukabidhi kutumia kwa ajili ya utukufu wake. Ustaarabu wowote ulianza baada ya ugunduzi na matumizi makubwa ya maliardhi. Ambako matabaka na uwajibikaji katika jamii uliongezeka, mahitaji yakaongezeka, uzalishaji ukahitajika zaidi. Lakini migangono ya kijamii ikashika kasi pia. Kwa kutafakari: unafikiri vurugu, maandamano, changamoto tulizonazo watanzania leo, zinatokana na nini?
         
Uzao wa Sethi
          Sasa tugeukie upande wa pili, uzao wa Sethi (4.25-5.32). habari njema katika Agano la Kale ni kwamba, mwanzo mpya ni sehemu ya njia ya kumtukuza Mungu baada ya kuacha yalokwisha pita. Kaini kama mzaliwa wa kwanza wa Adam na Hawa alishindwa kurejea kusudi la Mungu. Hivyo kuifanya jamii yake kuwa imara katika tamaduni na kushindwa kufikia malengo ya kijamii. Mungu akampa Hawa mwana mwingine, Sethi, kwa ajili ya nafasi ya Abel aliyeuwawa na kuanza kuchukua nafasi yake ya kurejesha uhusiano na upatanisho.[9]
          Jina la mwana wa Sethi, Enosh na babaye yanamaana ya ‘mtu’.[10] Mungu ana anzisha uzao mpya kupitia mtu mpya, Enosi. Katika kipindi cha uzao wa Enosi, watu walianza kuliitia jina la Mungu (mst. 26). Kwa kutumia ibada na sadaka wakajihusisha kumtafuta na kumpendeza Mungu. Kwa ujumla swala la dini lilianza kuchipuka na kukuwa hasa katika kipindi hiki cha Enosi.
          Mwanzo 5.2, kunakujirudia kwa maneno yaonyeshayo umuhimu wa mwanadamu kama wa pekee katika uumbaji. Adam anatajwa na wanae pia (mst.3), kwamba wanafanana naye. Sura na mfano wa Mungu haikutokea tena kwa wana wa Adam, bali wao walifanana na baba yao kwa sura na mfano.
          Jina Sethi lina maana ya ‘kuchukuwa nafasi ya.., Sethi alichuwa nafasi ya Kaini. Ambaye ndiye baba wa Mahelel amsifuye Mungu (mst. 12). Jaredi ‘shuka chini’ au mtumwa. Enoko ‘umepewa’. Metusela,  mtu wa shelah[11],  Nuhu, faraja, pumziko; Shem, jina. Ham, joto. Jafeti, Mungu akuongeze.
          Sethi alikuwa na wana wa kiume na kike. Watoto wa kike katika tamaduni ya kiyahudi hawakuwa na nafasi sawa na wakiume. Vile vile walipewa kipaumbele zaidi watoto wa kwanza walio wakiume kuliko wengine wote.
          Enoko alifanya tofauti na watu wengine: alitembea na Mungu (mst. 24). Enoko aliishi miaka 365 ambayo ni sawa na mzunguko wa majira ya mwaka. Jambo la muhimu hapa kufahamu ni uthamani wa maisha yake zaidi ya muda alioishi. Enoko na Nuhu ndio pekee walihesabiwa kutembea pamoja na Mungu. Walikuwa na nafasi ya muhimu katika kutengeneza mahusiano na Mungu. Tena wazi mahusiano na Mungu kama kutembea pamoja naye linajitokeza.

         


[1] Neville Carr, Purpose of Life (Sydney: Albatross Books, 1992), 4.
[2] Carr, Purpose of Life, 13.
[3] Carr, Purpose of Life, 16
[4] Davidson R., Genesis 1-11 (New York: Cambridge University Press, 1973), 4.
[5] Davidson, Genesis 1-11, 6.
[6] Davidson, Genesis 1-11, 6.
[7] Davidson, Genesis 1-11, 8.
[8] Carr, Purpose of Life, 16.
[9] Carr, Purpose of Life, 93.
[10] Carr, Purpose of Life, 93.
[11] Carr, Pupose of Life, 96.